Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Jumapili, tarehe 17 Agosti 2025, barabara za Mexico City zilijaa wananchi wa tabaka mbalimbali: Wanafunzi, wasanii, wanachama wa vyama vya wafanyakazi, wanaharakati wa kutetea haki za wanyama na hata baadhi ya viongozi wa serikali, wote wakishiriki katika maandamano haya. Msafara ulianzia katika Sanamu ya Malaika wa Uhuru na kupitia barabara kuu kama Paseo de la Reforma, Calle Juárez na Lázaro Cárdenas, kisha kumalizika katika uwanja wa kihistoria wa Plaza Tlaxcoaque.
Waandamanaji walibeba bendera kubwa za Palestina na mabango yenye kauli mbiu kama “Hii si vita, ni mauaji ya kimbari” na “Kuilinda Gaza ni Kuulinda Ubinadamu”. Walitoa wito wa:
- kusitishwa kwa mapigano mara moja,
- kutumwa kwa chakula na dawa Gaza,
- na kukatwa kabisa kwa uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, kijeshi na kielimu kati ya Mexico na Israel.
Mshiriki mmoja alisema: “Kuunga mkono Palestina ni kuunga mkono ubinadamu. Mateso wanayopitia yako nje ya fikra zetu.”
Maandamano hayo yaliandaliwa na makundi kama “Jukwaa la Kitaaluma na Kijamii kwa Palestina” na “Harakati ya Kimataifa kwa Gaza Mexico”, na yalihudhuriwa pia na Paco Ignacio Taibo II, Mkurugenzi wa Mfuko wa Utamaduni wa Kiuchumi wa Mexico. Akinukuliwa alisema: “Msiba wa Gaza ni aibu kwa ubinadamu. Mexico lazima iunge mkono wahanga, si watekaji.”
Waandamanaji walilaani pia uungaji mkono wa Marekani kwa Israel kwa njia za kijeshi, kifedha na kisiasa, wakikumbusha mauaji ya zaidi ya raia 61,000 akiwemo waandishi wa habari 269 Gaza. Walisisitiza kuwa msaada huu wa Marekani ndio unaoendeleza janga hilo.
Mojawapo ya sehemu kuu za maandamano ilikuwa Hemiciclo a Juárez, ambako kundi la “Wanazuoni kwa Palestina” walikuwa siku moja kabla wameweka ukumbusho wa upinzani uliopewa jina: “Palestina: Lango la Upinzani na Maisha”. Kumbusho hilo lina umbo la kivuli cha ardhi ya Palestina na maneno “Kutoka Mto hadi Bahari, Palestina itashinda”. Waandaaji walisisitiza kuwa hata kama utabomolewa, wataliweka tena.
Ingawa kulikuwa na misuguano midogo na polisi na kujeruhiwa kwa watu 11 (akiwemo mtu mmoja aliyeangukiwa na kipaza sauti na maafisa watatu wa polisi), maandamano kwa ujumla yalifanyika kwa amani. Polisi walidai baadhi ya waandamanaji walikusudia kufanya fujo na walikamata vifaa kama fimbo, minyororo na vitu vinavyoweza kuwashwa moto, madai ambayo waandamanaji walitaja kuwa ni jitihada za kukandamiza sauti zao.
Francis, mmoja wa wanaharakati, alisema: “Dunia inakumbwa na wimbi la ufashisti. Ukimya mbele ya jinai hizi ni ushirikiano.”
Zaidi ya maandamano, tukio hili lilikuwa ishara ya mshikamano wa kimataifa. Vikundi vilitangaza mipango ya kutuma meli za “Flotilla ya Uhuru” tarehe 31 Agosti kwa lengo la kuivunja mzingiro wa Gaza, ambapo Wamexico sita watashiriki. Walisema: “Hata meli moja ikifika Gaza, itafungua njia kwa zingine kufika.”
Your Comment